BARUA KWA BINTI WA 🇹🇿 #UZI
#PARTONE
Binti,
Salaam zikufikie pale ulipo kama upepo uvumavyo kutoka baharini kwenda nchi kavu. Natumaini hujambo. Mimi sijambo.
Kila siku nakuwaza sana. Nafikiria nifanyeje kugusa maisha yako.
Kabla ya yote nijitambulishe, mimi ni #DaktariMwandishi
Dhumuni la barua hii, ni kusema na wewe Binti. Natamani barua hii ningeiremba kwa maua, lakini naamini maneno nitakayoandika ni mbegu tosha.
Jana ilikuwa siku ya wapendanao, haijalishi ulipokea salamu au la, naomba pokea zangu; NAKUPENDA.
Enzi hizo nikiwa sekondari, ilikuwa siku
nzuri sana. Wale ma-admire/dada wa shule/vindende tuliandikiana kadi na kupeana zawadi. Ilipoangukia wikiendi kama hii, mambo yalikuwa moto zaidi, tulipokea kadi na barua kutoka kwa marafiki mbalimbali. Tukisubiria jumatatu tuibie kuingia facebook kuchungulia salam tulizotumiwa.
Natabasamu nikiandika hilo. Lakini kusudi langu sio kukupa stori yangu, ni kusema na wewe.
Natazama nyuma, nakumbuka vitu vingi nilivyosema, nilivyofanya, nilivyoandika na maamuzi mengi niliyofanya ambayo leo najiuliza "kwanini?"
Ni sehemu ya maisha.
Katika ukuaji wako, lazima
upitie haya. Katika safari yako, kuna vitu utavibakiza moyoni hutakaa useme kwasababu ni aibu. Kuna makosa utafanya. Si unajua? Unaanza kujiona umekua, unaweza fanya maamuzi yako, unatamani vitu kibao ukiona wenzio wanafanyiwa. Usiwe na tamaa. Niamini mimi, UTAVIKUTA. TENA VINGI.
JIPENDE. Upende mwili wako. Ipende afya yako ya akili. Katika ukuaji wako, kuna wakati unaweza kuuchukia mwili wako. Ngozi, umbo, sura, labda unatokwa na chunusi nyingi. Ni sehemu ya ukuaji, lakini usiruhusu ivunje kujiamini kwako. Nimepita huko. Nilipoumwa pumu ya ngozi,
niliharibika sana na kunenepa mno. Nilijichukia. Niliuchukia mwili wangu. Nilijiona sina mvuto. Imechukua miaka mingi kujifunza kujipenda tena. Nimetumia dawa nyingi kutoa makovu. Niamini, JIKUBALI. Wengi bado mna miili ya kitoto, usitake kuwa mtu mzima mapema. MUDA UTAFIKA.
Katika ukuaji wako, kitu kimoja hautaambiwa ni kuwa utavutiwa na wanaume. Tena wakati mwingine, watu wazima.
Si unajua, ukiwa Olevel wajanja wanatoka na wakaka wa Alevel, ukiwa Alevel, wajanja wanatoka na wakaka wa chuo. Ni ngumu kubadili hizi fikra ambazo zimeshajazwa kichwani
kwako, lakini niamini SIO UJANJA.
Ukiwa huko bweni, utamuona yule mwalimu kijana eeh, atakuvutia, utamchekeachekea labda, labda na yeye ataonyesha kukutaka pia. Vivyo hivyo utaenda jeshini, utamuona Afande, lile bakabaka, misuli utavutiwa. Nii kawaida, LAKINI kujenga mahusiano
SI SAWA. Wale ni watu wazima binti, si kila mtu mzima ana akili au aibu ya kukulinda wewe. Sikulaumu kama jamii inavyokulaumu kuwa "umejipeleka/umejitongozesha" lakini nakwambia JILINDE. CONTROL HISIA ZAKO.
Niamini mimi, ZINAPITA.
Kuna siku utatazama nyuma na kujicheka SANA kwa
kutamani hao.
Binti, bado jamii inatua gunia la misumari ya lawama kwa mwanamke. Tuna safari ndefu kuwajibisha wanaoharibu mabinti zetu. Wakati tunapigania hilo, naomba jilinde. Tumbo la mimba utabeba wewe mama. Magonjwa ya zinaa, majuto, aibu na masimango utapewa wewe.
KUWA MCHOYO. Kuwa mchoyo na kesho yako. Kuwa mchoyo na ndoto zako. Usiruhusu tamaa ya muda mfupi ibadilishe maisha yako.
Katika umri wako, bado hujaujua mwili wako, hujajua nini unapendwa kufanyiwa. Niamini mimi, muda UPO, utajua tu wakati ukiwadia. Utayafanya sana hadi upumzike.
Najua hili somo umeambiwa kwa maneno tofauti na wengi. Basi nasema hivi, ijue afya ya uzazi.
Ijue na uijue vema. Afya yako ya uzazi ni jukumu lako wewe peke yako.
Unapotimiza miaka 18, utakuwa na mipango mingi si kwasababu kisheria ndo umekuwa "mtu mzima" bwana? Naelewa. Amini.
Lakini kiukweli, hujawa mtu mzima. Nikukumbushe tu, hadi miaka michache iliyopita sheria ilikuruhusu uolewe ukiwa na miaka 14 kwa ruhusa ya mzazi. Sheria haimaanishi ni ukweli wa kiakili au kibaiolojia. Nini kinakufanya ufikiri kuwa ndani ya sekunde, siku, miezi ya kufikisha 18
ghafla umekuwa na utashi wa kiutu uzima. Wengi tumefanya makosa katika umri huo. Tumefanya maamuzi mabaya. Wengine hayakutudhuru, wengine yaliwadhuru. Jamii itakuaminisha "ushakuwa mtu mzima", lakini niamini, bado. Bado unahitaji kukua na kujifunza mengi.
Jifunze kwa makosa YETU.
Mengine utayarudia najua, lakini jitahidi mengi usiyarudie.
Dunia haijali binti, picha na video zinapovuja, lawama utabeba wewe na mama yako. Hata kama kuna mtu mzima mwenye makosa, jinsia yako itabeba lawama. Usirudie makosa YETU.
Tutasimama nawe katika safari yako, USITUANGUSHE
You can follow @Kudu_ze_Kudu.
Tip: mention @twtextapp on a Twitter thread with the keyword “unroll” to get a link to it.

Latest Threads Unrolled:

By continuing to use the site, you are consenting to the use of cookies as explained in our Cookie Policy to improve your experience.